Sheria za upigaji kura 30-06-2007.

Monday 18 June 2007
Wanablogu na wadau wote, baada ya kukaa na kutafuta njia muafaka ya upigaji kura wa haki na halali, uongozi wa muda umekubaliana kwamba uchaguzi utafanywa kwa kufuata sheria zifuatazo:-

1. Kura zitapigwa kwa kutumia blogu hii kwa kupitia kidirisha cha maoni.

2. Wapiga kura ni wale wenye blogu tu, hakutakuwa na 'anonymous' hii itasaidia kudhibiti
yeyote atakayetaka kupiga kura zaidi ya mara moja.

3. Siku ya kupiga kura, maoni yote yatafichwa hadi uchaguzi utakapokwisha, hii itasaidia
kufanya mpiga kura asibadili mawazo na kumpigia mtu mwingine, baada ya uchaguzi kura
zote zitawekwa wazi. (comment moderation itatumika.)

4. Viongozi wa muda ambao wamegombea nafasi za uongozi hawatasimamia upigaji kura.
Kutakuwa na wasimamizi wengine.

Bado haijajulikana muda kamili wa kupiga kura, kwa hili tunaweza kujadiliana wote.

Asanteni.
 
© Blogu Tanzania | Tarehe: 6/18/2007 |

Maoni: 12

  Tarehe: 18 June 2007 at 11:03 Blogger Mkina Anasema:
Kwanza kabisa nawapongeza viongozi wa muda kwa kuwa makini katika kuwasiliana nasi mapema na kutujulisha namna ya kupiga kura.
Ningependekeza muda wa kupiga kura uwe saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00 kwa majira ya huku kwetu Tanzania.
Zaidi ya mapendekezo yangu, nawaombeni wote KURA ZENU zenye thamani kubwa ili nipate kushiriki katika kuimarisha jumuia yetu, yenye kila sababu ya kukua na kuchangia kuleta mabadiliko ya jamii yetu kwa kuruhusu mawazo, maono, mtazamo na maoni huru kabisa yenye kujenga.
Kila jema na uchaguzi huru na wa haki.
Tuko pamoja.
  Tarehe: 18 June 2007 at 19:02 Anonymous Anonymous Anasema:
Nawapongeza viongozi wote wa muda kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhakikisaha jumuiya hii inasimama.
Nimeupata muongozo wa sheria itakayotumika kupiga kura,binafsi sijaridhishwa na kipengele cha pili,kuwa watakaopiga kura ni wale walio na blogu pekee na sio anonymous.
Kimsingi kama tunakubaliana kuwa JUMUWATA ni yetu wote hata wasio na blogu basi hata wasio na blogu wenye upenzi na blogu ni wanachama na wana HAKI ya kupiga kura.
Utaratibu huu hautendi haki, wapo wapendao kuwa na blogu zao lakini hawana na ni wanaharakati wazuri wa mtandaoni.Kutokuwa na blogu na kuziendesha kwa ufanisi mara nyingine inatokana na sababu za kiuchumi.Ndio maana kina 'ananymous' wataendelea kuwepo.Wana haki tusiwabague.
Je JUMUWATA ni jumuiya ya 'wenye nacho' pekee?
Ushauri wangu ni kwamba tusiwatenge.Utaratibu huu umekaa kibaguzi zaidi na unaingalia jumuiya kwa jicho moja tena la kushoto.
Viongozi wa muda naomba sheria ya uchaguzi ipitiwe upya.
La sivyo tuelezwe wazi kuwa wana JUMUWATA ni wenye blogu pekee.
Pendekezo
Viongozi wa muda mnaweza kuandaa utaratiu ufuatao:-
Kutoa muda maalumu kwa wana jumuiya wasio na blogu(wawablo)kujiandikisha na wapatiwe namba za siri ili wazitumie kwenye uchaguzi.
Moja ya mambo muombaji atakayo takiwa awakilishe kwa kamati ni pamoja na e mail yake na jina lake kamili.
Endapo itaonekana haiwezekani basi wale wasio na blogu wajiorodheshe ili wajuzi wa mambo wawatengenezee blogu, kama ndugu MK alivvyo wasaidia wengi kuwatengenezea blogu.
Kama JUMUWATA ni ya wenye blogu pekee basi litakuwa ni jambo jema,itakuwa imeongeza wanachama
Itoshe tu, kusema kwamba sheria hii haifai na inabagua baadhi yetu.
Tufanye vyovyote kuhakisha kila mmoja wetu anaitumia haki yake ya kidemokrasia.
Nitafurahi kupata ufafanuzi mapema kutoka kwa viongozi wa muda.Tarehe 30/6/2007 sio mbali.
Naomba kuwasilisha.
Wadau mnasemaje?
Pius
Pius,
Kwanza kabisa tunapenda ijulikane kwamba jumuiya tunayoiunda ni jumuiya isiyo na ubaguzi wa aina yoyote ile. Pili kama tulivyoeleza hapo awali kuhusu nani apige kura, nia ni kutaka kudhibiti waharibu kura na si kuwatenga wengine, tunashukuru kwa wazo lako ni zuri sana tunalifanyia kazi.

Wakati huo huo kama kuna yeyote anayedhani ana njia yoyote ya kusaidia kufanya uchaguzi kuwa wa haki na huru tunaomba asisite kutoa wazo lake, tukumbuke uchaguzi huu ni wa mtandaoni hivyo tunahitaji njia madhubuti kuhakikisha mambo yanaenda vizuri.

Pius tunashukuru kwa wazo lako.
  Tarehe: 19 June 2007 at 07:51 Blogger luihamu Anasema:
NANUKUU
jumuiya wasio na blogu(wawablo)
kujiandikisha na wapatiwe namba za siri ili wazitumie kwenye uchaguzi.

Ningependa kuaanza kwa kusema JUMUWATA HAIBAGUI,KAMWE HAITA BAGUWA.

Hawa ndugu zetu wasio na blogu tunawajali sana na kukaribisha maoni yao lakini hawa ndugu zetu hata kama kamati ya muda ikiamuwa kutoa namba za siri hazitasaidia kwasababu zifwatazo.

1.anonymous ni wengi na wanaweza kujirudiarudia,anonymous mmoja anaweza kuwa na majina zaidi ya kumi na email zaidi ya thelathini,je kamati ya maandalizi inavifaa vyakuweza kutambua anonymous kwa jina la LUIHAMU RINGO hata jiandikisha kwa mara ya pili kama CHEDIEL CHARLES?

2.Uraia,je kamati ya maandali itakubali kupokea kura kwawale ambao si rai wa TANZANIA KATIKA UCHAGUZI HUU?Hawa ndugu zetu anonymous wanatoka nchi tofauti tofauti,sasa kamati ya maandalizi inavifaa vya kutambua anonymous Luihamu Ringo ni Mtanzania au Mwingereza?

3.Swala la kutoa namba kwa kila anonymous halita saidia vilevile, kwasababu anonymous Luihamu Ringo anaweza kupata namba zaidi ya mara hamsini.kwa mfano.

utambulisha wangu unaweza kuwa hivi.

Jina la anonymous Luihamu Ringo
namba ya kupiga kura 15
email itoi@yahoo.com

vile vile huyu huyu anonymous Luihamu Ringo akajiandikisha tena kwa jina la

jina anonymous Chediel Charles
namba ya kupiga kura 20
email charles10@yahoo.com
n,k.

Kamati ya maandalizi muwe macho.
HUU NI MTAZAMO WA RASTA.
NUFF NUFF RESPECT.
Demokrasia ni nadharia ngumu sana katika utekelezaji wake, mtekelezaji wa demokrasia anatakiwa kuangalia pande zote za 16 za dira na hapo ndipo unapokuja ugumu katika utekelezaji wa nadharia ya demokrasia. Ndio maana nadharia ya udikteta pia huwa inachukuliwa kama njia mbadala katika utekelzaji wa jambo husika.

Kuwazuia 'anon's' kupiga kura ni udikteta lakini hiyo naamii demkrasia kwa wanablogu wenye blogu na sababu zangu hazitofautiani na ndugu yangu katika imani Ras Luhaimu.

Demokrasia na Udikteta ni ndugu hasi kutoka damu chanya.

Naomba kuwasilisha!!
  Tarehe: 19 June 2007 at 17:54 Anonymous Anonymous Anasema:
Luiamu na DaMija
Nilikuwa natafuta maneno ya kusaidia point ya daMija, lakini naona Luiamu umejibu vizuri sana.
  Tarehe: 19 June 2007 at 18:53 Anonymous Anonymous Anasema:
Da'mija nashukuru kwa ufafanuzi.Napata picha ya kiongozi atakiwaye, asiye na mawazo yaliyoganda.Jibu ulilolitoa linaakisi picha ya kiongozi bora.Si lengo langu kukufagilia, ingawa unastahili.Ni vyema tukajaribu kutoa hoja zinazokidhi na kujibu hoja ipasavyo.Si busara kutoa jibu jepesi kwenye suala gumu linalohitaji tafakuri kwa faida pana zaidi ya jumuiya..Da'mija umeahidi kulitafakari na viongozi wa muda.Bado nina matumaini na ninasubiri jibu.Nahisi ninatoa sauti ya kina anonymous wengine pia.
Nilichohoji hapo awali ni kuwa, kama JUMUWATA ni yetu sote yaani wenye blogu na wasio na blogu kwa nini usitafutwe utaratibu wa kuwashirikisha na wasio na blogu.Na kuhakikisha hakuna kura itakayopotea wala kuibiwa?.Hii ni changamoto. Michango iliyotoka kwa wagombea bila shaka inasukumwa na hofu ya kuibiwa kura katika uchaguzi.
Luihamu, Kaka Pori na Mirium wasio na blogu hawana haki?, je jumuiya hii ni yenu 'wenye blogu' pekee. Kwa nini msitoe mawazo muruwa ya kuwashirikisha wasio na blogu, kina 'anonymous'. Nilieleza kuwa kama jimuiya hii ni ya wenye blogu pekee basi kamati ya muda ipokee maombi ya wapendao kuwa wanachama kwa kuwasidia kujenga blogu zao wenyewe.Huu ndio ubunifu na sio mawazo mgando ya kuruhusu demokrasia dhaifu JUMUWATA na kuushabikia udikteta.Wajuzi wa masuala ya teknilojia hii wanaweza kufanya kazi nzuri kama aliyoifanya MK kwa wengi wa walio na blogu.Kama tunasema kadi ya mwana jumuiya ni 'kuwa na blogu yake',itamkwe kuwa kadi ya uanachama wa JUMUWATA ni blogu.Kama atakayechaguliwa ni kiongozi wangu kwa nini nisishiriki kumchagua?
Binafsi ni msomaji mzuri wa blogs zenu.Simon alipata kuandika ni vyema pakawa na viongozi watakaoipa nguvu jumuiya kipindi hiki imevaa nepi.Wenye ubunifu. Narudia niliposimamia awali, sheria hii ya uchaguzi inabaguwa na haifai, ipitiwe upya,hata maneno mazuri kiasi gani yangetumika kuipitisha na kuitumia.
Walio nje wanaotaka kuingia ndani, wasitengwe, wakaribishwe.
Pendekezo:-
Wigo wa wanachama upanuliwe kama kigezo ni kuwa na blogu,yaani kadi ya uanachama ni blogu,sisi kina anonymous tusaidiwe kupata kadi za uanachama kwani tunapenda kuwa ndani ya jumuiya, naomba tusitengwe.Kina anonymous watangaziwe offer ya kutengenezewa blogu, nawahakikishia idadi ya watanzania wenye blogu itaongezeka.JUMUWATA itakuwa na nguvu.
Kama nasi tuna nafasi katika jumuiya naomba tutengezewe utaratibu wa kuchagua viongozi.
Naomba kuwasilisha.
Pius
Pius,
Kama nimekuelewa vizuri ni kwamba ungependa sana kuwa na blogu lakini hujui jinsi ya kufungua. Usihofu kaka yangu, kufungua blogu ni rahisi kupita kufungua email adress. Nakuomba ufungue www.blogger.com halafu hapo fuata masharti yote nakuhakikishia utakuwa na blogu yako si chini ya dakika tano.

Pius, nia ya jumuiya hii ni kuongeza haraka iwezekanavyo idadi ya wenye blogu na hatua ya kwanza tunayoichukua kulitekeleza ni hii ya sasa hivi ya kuwataka watu waanzishe blogu ili kuweza kupiga kura.

Mwisho, baada ya kufungua blogu yako, naomba ugombee nafasi ya uongozi nafasi za lala salama bado zipo. Nasubiri maelezo yako niyaposti.
  Tarehe: 20 June 2007 at 07:38 Blogger luihamu Anasema:
Nanu kuu,
Michango iliyotoka kwa wagombea bila shaka inasukumwa na hofu ya kuibiwa kura katika uchaguzi.
Luihamu, Kaka Pori na Mirium wasio na blogu hawana haki?, je jumuiya hii ni yenu 'wenye blogu' pekee.

Ndugu Pius naomba nikujibu kwa niaba ya Miriam,Kaka Poli.anonymous wote wanahaki duniani ya kushiriki katika swala lolote kama hili la uchaguzi lakini kuna taratibu za kupiga kura.

Naomba kuwauliza anonymous wote walikuwa wapi wakati wa mada kuhusu kujenga jumuiya hii ya JUMUWATA,kamati ya maandalizi ilikuwa inatoa wiki moja na siku kadhaa kama kuna swala ambalo halijakamilika,kama mngeshiriki katika mada hizo naamini tatizo lenu lingekuwa limetatuliwa zamani.

Mzee Ndesanjo kaandka utaratibu wa kuanza kublogu katika blogu yake na pia kwenye vyombo vya habari kama vile GAZETI LA MWANANCHI,akaelezea jinsi ya kuanza kublogu au nadanganya?

Mimi mwenyewe nilipata habari kuhusu kublogu katika makala ya Mzee Ndesanjo anazoziandika katika gazeti la Mwananchi nikafwatilia kwa makini akanisaidia,baada ya hapo Mzee Ndesanjo akaniagiza kwa MWANABLOGU RAMADHANI MSANGI AU MSANGI MDOGO akanisaidia leo hii blogu yangu imetengenezwa na MK yule Mkuu wa MAHUSIANO.COM.

Sasa naomba tujiulize,kama mtu usipojituma inakuwa vigumu kidogo hembu fikiria Mk yuko Uingereza lakini nilijitahidi kuwasiliana nae na akanitengenezea blogu yangu.

Niliandika katika blogu yangu swala la kumomba Mk atutengene Blogu na nikawasiliana na Mk akaniambia yeye hanatatizo na atatengeneza blogu bila wasiwasi.

Kwa kumpata Mk kwa haraka wasiliana nae kupitia Yahoo Messenger atakusaidia Ndugu yangu Pius

Mtafute kwa jina la akathepretender na kama hayuko online acha messeng.


Nuff Nuff Respect.
  Tarehe: 20 June 2007 at 14:32 Anonymous Anonymous Anasema:
Maelezo ya Luihamu naona yameeleza kwa kina jinsi ambavyo itakuwa vigumu kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa haki iwapo mtu yeyote asiyetambulika ataruhusiwa. Na kwa teknolojia tuliyonayo hivi sasa katika jumuiya yetu ni vyema zaidi kutoruhusu wasio na blogu au wasiotumia majina yao kupiga kura. Sio kuwa tunabagua ila ndio njia bora tunayoiona inaweza kutumika hivi sasa. Ila kama kuna mawazo zaidi basi yanakaribishwa.
  Tarehe: 20 June 2007 at 19:25 Anonymous Anonymous Anasema:
Majibu mazuri sana, kuhusu kina anonymous kushiki kupiga kura.Nakubaliana na wote Damija, Ndesanjo na Luihamu.Nahisi kipengele cha pili cha sheria itabidi kisomeke vizuri kuonyesha tu ingawa kina anonymous hawaruhusiwi kupiga kura nao wanahitajika ndani ili wapige kura.
Maelezo ya jinsi ya kuanzisha blogu huenda yakasaidia sana, naamini kuwa tutakaoanzisha hatutaishia kupiga kura tu na kusubiri uchaguzi ujao tutayaendeleza yale yote yaliyo mema yatakayotuwezesha kupiga hatua mbele kama wanajumuiya na kama watanzania.
Hivi karibuni ntawakimbia kina anonymous,nitaanzisha blogu yangu.
Damija, kuhusu kugombea nahisi nitaongeza idadi ya wagombea tu, na lengo ni kupata kiongozi.Hivyo lengo halitatimia,lakini tuko pamoja.
Nimefurahi mmeyafanyia kazi mapendekezo.
Ndesanjo kakaribisha mawazo. Ninayatoa kama ifuatavo:-
Ili tusonge mbele kwa kasi kuna haja ya kutangaza yanayoendelea nje ya humu ndani ili walio nje nao wapate taarifa na washiriki.Wapo wasioingia humu ila wanapita kwingine.Hivi kuna tatizo lolote kutumia blogu kama ya MICHUZI kueleza JUMUWATA ni nini?, Nani anaweza kujiunga na JUMUWATA, yaani sifa ya wanajumuiya kama hiyo iliosemwa ya kuwa na blogu.
Na kuunganisha na jinsi ya kuanzisha blogu ili kupata sifa ya kuwa mwanachama na kupata haki zote za wanachama ikiwemo kupiga kura na kushiriki yote yahusuyo jumuiya.Nasema hivi kwa kuwa wote tunajua Jumba la Michuzi linatembelewa na wengi, hivyo taarifa zitawafkia wengi, walio ndani na nje ya Tanzania.
Nahisi kuna haja ya kuitangaza zaidi
Isije ikatokea wagombea wanane wapiga kura wanane.Tuwahamishe wadau waingie ndani tuicheze ngoma.
Pius
Mtaniwia radhi kama nawarudisha nyuma kiasi, nimeona niulize swali kuwa je naweza kuwa mwanachama na ni zipi taratibu.

ahsante.

YAKUBU