Tafakari na changia kuhusu Kamati za JUMUWATA

Tuesday 11 September 2007
Kuna umuhimu wa kuzipitia hizi kamati na kuchangia maoni yakuzijenga au hata kuzibomoa.

Tunahitaji kuzijenga hizi kamati ili kurahisisha ufanyaji kazi wa JUMUWATA. Itasaidia kuwezesha shughuli kuenda muruwa. Lakinni kabla ya kuzianzisha tunahitaji maoni ya kuziweka zijengeke vyema.

Kumbuka kuanzia jina la kamati laweza kubadilishwa ukiwa na hoja ya kulisahihisha.

Changia hata kamati mpya kama unafikiri inahitajika.

Angalia hizi hapa chini halafu changia .

a. Kamati ya harakati

Kamati ishughulikiayo utangazaji na upelekaji wa elimu na mafunzo yawafaayo wananchi yapatikanayo katika blogu za JUMUWATA kufikia jamii. Kamati hii itashughulikia miradi itokanayo na Jumuwata kufanyiwa kazi katika maeneo yagusayo jamii moja kwa moja .(Mfano :kutoa mafunzo madarasani na katika jamii kwa njia ya uso kwa uso au kwa kutumia vitabu,pamfleti,videonk.,kuhudumia watoto wa mitaani, kuhamasisha usafi, kupanda miti nk.).

b. Kamati ya Ufundi na teknolojia
Kamati hii huhusika na:
Ufundi utumikao kuboresha blogu na pia mambo mapya ya teknolojia yawezayo kuboresha blogu za wanaJumuwata.
Itakuwa na majukumu ya kuwezesha mikutano ya JUMUWATA katika mtandao.
Kusaidi kushauri waanzao kublogu
Kutupa taarifa mpya za tekinolojia huru ambazo zitasaidia kuboresha blogu zetu
Kupeleka elimu ya blogs mashuleni nk ikishirikiana na kamati ya harakati.
Kutengeneza na kuhudumia kikusanya habari(aggregator)
Kuunda na kuimarisha tovuti ya jumuiya.
Kutoa elimu ya kutengeneza blogu kwa atakayependa






c. Kamati ya Mahusiano na vyombo vya habari.
Kamati hii itahusika na kujenga uhusiano wa Wanablogu wa JUMUWATA na vyombo vya habari, vya Tanzania na Dunia. Itahusika kuandaa habari muhimu ambazo JUMUWATA inapendelea ziwafikie Wananchi kwa kutumia vyombo vingine vya habari kama vile TV,na magazeti.Itahusika kuhakikisha jina la JUMUWATA halichafuliwi na vyombo vingine vya habari.



d. Kamati ya Maadili na Ubora wa Blogu (Kamati ya picha)

Kamati hii itashughulikia uboreshaji wa blogu za JUMUWATA hasa katika maswala ya matumizi ya picha na uboreshaji wa taaluma ya picha , video na mengineyo yahusuyo uboreshaji wa blogu ili kuzipa nguvu zaidi katika uelimishaji jamii na pia kurahisisha ujumbe kufikia jamii.

e. Kamati ya sheria na Utunzaji wa maadili ya JUMUWATA

Kamati hii huhakikisha kuwa sheria na maadili ya JUMUWATA yanafuatwa na wanaJUMUWATA. Pia hufuatilia na kuweka wazi maswala ya kisheria ambayo yanaweza kumkumba mwanablogu. Itahusika pia na kuandaa hatua za kuwaengua viongozi na wanajumuwata kama wanakiuka maadili na sheria zichungazo JUMUWATA.

f. Kamati ya uenezi na uhamasishaji

Kamati hii inashughulikia maswala ya kupata wanablogu wapya na kusaidia kuwaamsha wanablogu wanaolala na kuacha kublogu. Kamati hii itahusika pian a kuelezea manufaa ya kublogu kwa jamii.

g. Kamati maalumu ya uchaguzi

Kamati hii itashughulikia maswala yote ya uchaguzi wa viongozi wa JUMUWATA. Itahusika pia na mapendekezo ya uchaguzi wa miradi itakayotakiwa kupewa kipaumbele na JUMUWATA katika kipindi husika.
 
© Blogu Tanzania | Tarehe: 9/11/2007 |

Maoni: 3

Kamati zote zimetulia sioni kama kunasababu ya kuongeza kamati zingine.

N.b Licha ya muda kubana najitahidi kuchangia.

AMANI.
Nimeangalia KAMATI YA MAHUSIANO NA VYOMBO VYA HABARI na KAMATI YA UENEZI NA UHAMASISHAJI nimeona kama vile shughuli zao zinaweza kuwa pamoja...au?
Kamati zimetulia.Kama alivyosema bwana Ndabuli na mimi nimeona kama KAMATI YA MAHUSIANO NA VYOMBO VYA HABARI na ile ya UENEZI NA UHAMASISHAJI kazi zake zinaelekea kufanana.

Mapendekezo yangu kwanini wakuu msiweke iwe kamati moja....labda tuiite KAMATI YA UEZENI NA UHAMASHAJI.

Wajumbe wenzangu mna maoni gani kwa hilo?

-->Idumu JUMUWATA