Endelea kupitia dondoo hizi, chambua, kosoa, ongezea, kemea , ili tupate kitu cha uhakika.......Dondoo ni hizi hapa .Zimepandishwa kutokana na baadhi yetu kushindwa kufungua faili hapo chini.Tuko pamoja!KATIBA YA JUMUIYA YA WANABLOGU TANZANIA
Katiba ya JUMUWATA 2007
UTANGULIZI
Sisi WANAJUMUWATA tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga jumuiya yetu tukizingatia misingi ya uhuru, haki na amani. Misingi hii itaweza kutekelezwa katika JUMUIYA iendeshwayo kidemokrasia ambapo uongozi wa jumuiya na wanachama wa jumuiya wanashirikiana katika kudumisha haki zote za binadamu, maadili ya mjengayo mwanadamu kufanya mazuri na kuendelea na uhuru wa habari .
Katiba hii imetungwa kwa ushirikiano wa WANAJUMUWATA wote, kwa dhumuni la kujenga Jumuiya ya wanablogu wenye nguvu ya kubadili mapotofu, kuweka wazi yaliyofichika, kuelimishana, kuburudisha na kujikwamua katika mipaka izuiayo uwezo wa mwanadamu kupata uwanja wa kusemea na kusikika duniani.
* SURA YA KWANZA
SEHEMU YA KWANZA
JUMUIYA YA WANABLOGU TANZANIA.
Ni jumuiya iunganishayo Wanablogu wenye blogu na wasio na blogu popote duniani, ambao madhumuni yao ni kuendeleza Tanzania kama nchi, Watanzania na Dunia kwa ujumla. Ni jumuiya isiyoendeshwa kibiashara , yenye lengo la kumfaidisha mwanablogu na Mtanzania mwenye kupenda maendeleo.
1.Maeneo JUMUWATA igusayo.
JUMUWATA inagusa wanablogu dunia nzima, na maeneo yote yamgusayo binadamu ,kwa nia ya kumjenga, kumelimisha, na sio kumdhalilisha. JUMUWATA haikubaliani na mwanablogu yeyote mwenye nia ya kubomoa utu wa binadamu mwingine asiye na hatia.
2.Nani ni MwanaJUMUWATA.
MwanaJUMUWATA ni mtu yeyote, kikundi chochote chenye nia ya kujenga mazuri yagusayo Tanzania na dunia kwa ujumla, kitambuliwacho na kusajiliwa na JUMUWATA, na kufuata sheria na maadili yakubaliwayo na JUMUWATA.
Blogu na wanablogu wakubaliwao na JUMUWATA
Mtanzania yeyote mwenye blogu na asiye na blogu mwenye kukubaliana na maadili na sheria za JUMUWATA.
Mwanablogu yeyote duniani apendaye maendeleo ya Tanzania na kukubaliana na maadili/sheria za JUMUWATA
3.Uongozi wa JUMUWATA
Uongozi wa JUMUWATA uko katika ngazi tatu.
1.UONGOZI Mkuu (Mwenyekiti ,Katibu na Mweka Hazina)
2. Uongozi Kamati (Uongozi ushirikishao wanakamati wote).
3. Uongozi Mwanachama. (Huu ni uongozi umhusuo mwanajumuiya yeyote katika JUMUWATA.Tunaamini kuwa mwanablogu yeyote ana haki ya kuongoza na kusikilizwa katika JUMUWATA katika maswala ambayo yanafaidisha JUMUWATA na mwanadamu kwa ujumla.
Uongozi mwanachama utatambulika pale tu kikao kihusichasho Wanajumuwata , Uongozi Mkuu na Uongozi Kamati kitakubali kuwa jambo husika litaongozwa na Uongozi Mwanachama.
4.Kamati ziwakilishazo JUMUWATA
a. Kamati ya harakati
b. Kamati ya Ufundi na teknolojia
c. Kamati ya Mahusiano na vyombo vya habari.
d. Kamati ya Maadili na Ubora wa Blogu (Kamati ya picha)
e. Kamati ya sheria na Utunzaji wa maadili ya JUMUWATA
f. Kamati ya uenezi na uhamasishaji
g.Kamati maalumu ya uchaguzi
SEHEMU YA PILI
MALENGO MUHIMU NA MISINGI YA MWELEKEO WA JUMUWATA
5. Ufafanuzi
Lengo kuu la JUMUWATA ni kuwezesha wananchi wa kawaida kuwa na uwezo wakufikisha na kupokea ujumbe bila kufungwa na ukiritimba uliojengeka katika vyombo vingine vya habari. Inanuia kujenga jumuiya imara ya wanablogu ambao watakuwa ni mchango kwa maendeleo ya jamii kupitia uwezo wao wakuanika ujuzi na mawazo yao katika blogu zenye kuvutia na zenye ujumbe ujengao. Kuwezesha kublogu kwa ajili ya maendeleo ya jamii ni moja ya lengo kuu la JUMUWATA.
6.Shughuli za JUMUWATA
* JUMUWATA inaunganisha wanablogu wapenda maendeleo ya Tanzania na dunia kwa ujumla. Wanajumuwata wanaamini umoja ni nguvu na jumuwata ni chombo cha kuunganisha nguvu za wanablogu kwa nia yakupiga hatua mbele, kimaendeleo, kifikira na kiubinadamu.
* Jumuwata kwa kupitia nguvu za wanajumuwata, itaendesha miradi itokanayo na fikira na busara zitolewazo katika blogu za JUMUWATA, ilikugusa na kujenga jamii pale ilipo.(Mfano miradi igusayo jamii kwa njia ya vitabu, miradi isaidiayo watoto yatima, miradi ya kuhamasisha jamii kupata njia za kutatua matatizo yao, nk.)
* Kuwapamotisha Watanzania duniani kote kujishughulisha kifikira na kwa uwezo wao wowote kusaidia miradi ya kusaidia Tanzania.
* Kuwezesha wanablogu wa Tanzania kusikika katika jamii.
7.Kuitangaza JUMUWATA
Ni jukumu la kila mwanajumuwata kuitangaza JUMUWATA. Blogu za JUMUWATA zinatakiwa kuweka nembo ya JUMUWATA. Vyombo vya habari kama magazeti, luninga nk ;havitasahaulika katika kutangaza JUMUWATA.
8.Utekelezaji wa shughuli za JUMUWATA
Shughuli za JUMUWATA zitatekelezwa kupitia uongozi wa JUMUWATA, kamati za JUMUWATA, na wanachama wa JUMUWATA kwa kushirikiana.
SEHEMU YA TATU:
HAKI.
7.Haki za wanaJUMUWATA
Wanajumuwata wote ni sawa. Mwanajumuwata yeyote ana haki ya kutoa mawazo na kukosolewa katika JUMUWATA. Mwanajumuwata yeyote mwenye umri zaidi ya miaka kumi na nane anahaki ya kuwa kiongozi wa JUMUWATA.
8. Haki ya kupata elimu na kuelimisha katika JUMUWATA
Tunaamini kuwa kila mwanajumuwata analo la kumfunza na lakujifunza kutoka kwa mwingine. Mwanajumuwata yeyote anahaki yakufunza na kufunzwa katika JUMUWATA.
9. Haki ya kutamka,uhuru wa mawazo na kuwa na sauti ndani ya JUMUWATA
Mwanajumuwata anahaki ya kutamka lolote na kuwa na sauti ndani ya JUMUWATA iwapo tu haki hiyo haitumiki kumtukana mtu, kujenga ubaguzi wa rangi ,umri , jinsia nk. Haki ya kutamka, uhuru wa mawazo na kuwana sauti ndani ya JUMUWATA itaheshimika tu pale itumikapo kujenga na sio kumdhalilisha mtu au watu kwania ya kujenga chuki na sio kujenga jamii bora.
10.Haki ya Kuongoza , na kukataa Uongozi wa JUMUWATA
Kila mwanajumuwata ana haki ya kuongoza na kukataa kuongoza. Kila mwanajumuwata ana haki ya kuukataa uongozi, haki ambayo anaweza kuifikisha kwenye kamati maalumu ya sheria na utunzaji wa maadili, kwa kujadiliwa na mapendekezo zaidi yashirikishayo wanajumuwata wote.
SEHEMU YA NNE:
WAJIBU
11.Wajibu wa kushiriki katika shughuli za JUMUWATA
Ni wajibu wa kila mwanajumuwata kushiriki katika shughuli za JUMUWATA kama zipendekezwavyo na JUMUWATA.
12.Wajibu wa kutii sheria za JUMUWATA.
Ni wajibu wa kila mwanaJUMUWATA kutii sheria zilizokubaliwa na JUMUWATA ambazo zimepitishwa kwa kushirikisha maamuzi ya wanajumuwata wote.
13.Wajibu wakulinda mali za JUMUWATA
Ni wajibu wa wanajumuwata kuwa na uchungu na mali za JUMUWATA na kuzilinda . Adui wa mali za JUMUWATA aliye ndani au nje ya JUMUWATA ni adui wa wapenda maendeleo ya JUMUWATA.
14.Wajibu wa kulinda sifa nzuri ya JUMUWATA.
Ni wajibu wa kila mwanajumuwata kuzilinda sifa nzuri za JUMUWATA. Ni wajibu wa JUMUWATA kusaidia kuondoa au kubomoa yale yawezayo kuletea JUMUWATA sifa mbaya.
SEHEMU YA TANO:
15. MAMBO YA KUZINGATIA KWA MWANAJUMUWATA
a. Gharama za JUMUWATA hazitamuathiri mwanajumuwata binafsi katika maswala yahusuyo kushitakiwa JUMUWATA , kudaiwa fedha kutokana na shughuli za JUMUWATA
b. Kiongozi wa JUMUWATA hata daiwa binafsi kulipia shughuli zilizopitishwa kikatiba na wanajumuwata kwa kukubaliana.
c. Kiongozi wa JUMUWATA atadaiwa akitumia mali za jumuwata kiuzembe na kwa makusudio binafsi
d. Kiongozi mpya wa JUMUWATA hatahusishwa na mapungufu ya fedha na mali za jumuwata yaliyotokea kabla ya kushika kwake uongozi.
e. Katiba hii inatakiwa kufuatwa na yeyote atakaye kujiunga na ambaye ni mwana JUMUWATA
f. Atakayegundulika kwenda kinyume na maadili ya JUMUWATA , atapewa onyo na kuombwa ajitetee.Hatima itakuwa ni kuondolewa katika JUMUWATA kwa kipindi kitakacho amuliwa na wanajumuwata.
g. Mwanajumuwata atolewaye kwenye jumuwata atatakiwa arudishe mali zozote za JUMUWATA ikiwa ziko mikononi mwake.
* SURA YA PILI
MUUNDO WA JUMUWATA
SEHEMU YA KWANZA:
MWENYEKITI
16. Mwenyekiti wa JUMUWATA
Ni kiongozi mkuu wa maswala yote yahusuyo JUMUWATA.
17.Shughuli za Mwenyekiti katika JUMUWATA
* Atasimamia vikao vyote vikuu vya JUMUWATA .Anaruhusiwa kuingia katika vikao vyote vya kamati za JUMUWATA iwapo wanakamati hawana kipingamizi.
* Anawakilisha maswala yote ya JUMUWATA ambayo hakuna kamati maalumu inayasimamia moja kwa moja.
* Ni msemaji mkuu wa maswala yaihusuyo JUMUWATA.
* Ni wajibu wake kujua maswala ya uwezo wa JUMUWATA kifedha, kikuwakilisha wanajumuwata, nk.
* Ni muweka sahihi mkuu katika maswala na vyeti vyote vihusuvyo JUMUWATA.
18.Mamlaka na utekelezaji wa shughuli za Mwenyekiti
Mamlaka ya mwenyekiti huyapata tu pale ashindapo katika uchaguzi na kukabidhiwa uongozi rasmi. Utekelezaji wa shughuli za mwenyekiti unatakiwa uwe wazi kwa wanajumuwata.
19.Uchaguzi wa Mwenyekiti
Uchaguzi wa mwenyekiti utafanyika kwa kawaida pamoja na uchaguzi mkuu wa viongozi wengine.Uchaguzi wadharura waweza kufanyika pale Mwenyekiti ajiudhurupo au kutakiwa kujiengua kutokana na kukiuka maadili ya JUMUWATA.
20. Sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti
Mwenyekiti wa JUMUWATA ni mwanajumuwata yeyote mwenyeblogu atakayegombea , mwenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi. Mwenyekiti anatakiwa aonyeshe moyo wa kutaka kuendeleza JUMUWATA, Aonyeshe kuwa anauwezo wa kuendesha jumuiya.Ni yule atakayeshinda kwa kura halali za wanajumuiya.
21.Haki ya kuchaguliwa tena.
Mwenyekiti anahaki ya kugombea tena kiti hicho kihalali kama wanajumuiya hawana kipingamizi na wanaridhika na kazi aliyofanya.
22.Utaratibu wa uchaguzi wa Mwenyekiti
Uchaguzi wa Mwenyekiti utafuata taratibu za kawaida za uchaguzi wa JUMUWATA. Mwanablogu atakaye Uenyekiti, anahitajika kuwakilisha jina na picha yake . Atatakiwa ajieleze ni kwanini anafikiria yeye ni bora kuongoza JUMUWATA. Baada ya hapo atasubiri upigaji kura kama utakavyoandaliwa na kamati maalumu ya uchaguzi. Wapiga kura ndio waamuzi wakuu katika uchaguzi.
23.Wakati na muda wakushika madaraka ya Uenyekiti.
Muda wa kushika madaraka ni miaka miwili.Mwenyekiti anawezakujiudhuru au kuenguliwa kwa mujibu wa katiba.
24.Masharti ya kazi ya Uenyekiti.
Mwenyekiti hataruhusiwa kuwa katika kamati ya uchaguzi iwapo ananuwia kugombea Uongozi tena. Ni mtunzaji mkuu wa JUMUWATA, hatakiwi kuigeuka JUMUWATA akiwa ofisini.
25.Kiapo cha Mwenyekiti wa JUMUWATA.
Mwenyekiti ataapishwa kwa kiapo cha kukiri kufuata katiba ya JUMUWATA.
SEHEMU YA PILI
KATIBU
26.Katibu wa JUMUWATA
Katibu wa JUMUWATA ni mtekelezaji mkuu wa maswala yahusuyo JUMUWATA.
27.Kazi na Mamlaka yake katika JUMUWATA
* Ni karani mkuu aratibuye maswala ya JUMUWATA.
* Atahudhuria vikao vyote vikuu vya JUMUWATA na kunukuu yote muhimu yawakilishwayo kikaoni.
* Ataletewa na kuhifadhi yaleyote yatakayo jadiliwa katika vikao vyote vya kamati za JUMUWATA.
* Ni mtunza rekodi za maswala yote yahusuyo JUMUWATA.
* Ataongoza vikao vya JUMUWATA ikilazimu akishirikiana na Muweka hazina iwapo Mwenyekiti hakuweza kuhudhuria.
* Anauwezo wakuwakilisha JUMUWATA kwa kuweka sahihi katika makala na vyeti vyote vihusuvyo JUMUWATA.
* Atashiriki katika maswala yote mengine atumwayo na Mwenyekiti au Vikao vya JUMUWATA , yasiyolengwa na kamati maalumu za JUMUWATA.
28.Uchaguzi wa Katibu
Uchaguzi wa katibu utafanyika kwa kawaida pamoja na uchaguzi mkuu wa viongozi.Uchaguzi wadharura waweza kufanyika pale katibu ajiudhurupo au kutakiwa kujiengua kutokana na kukiuka maadili ya JUMUWATA.
29.Sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Katibu
Katibu wa JUMUWATA ni mwanajumuwata yeyote mwenyeblogu atakaye gombea , mwenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi. Katibu anatakiwa aonyeshe moyo wa kutaka kuendeleza JUMUWATA. Aonyeshe kuwa anauwezo wa kuendesha jumuiya.Ni yule atakayeshinda kwa kura halali za wanajumuiya.
30.Haki ya kuchaguliwa tena
Katibu anahaki ya kugombea tena kiti hicho kihalali kama wanajumuiya hawana kipingamizi na wanaridhika na kazi aifanyayo.
31.Utaratibu wa uchaguzi wa Katibu
Uchaguzi wa katibu utafuata taratibu za kawaida za uchaguzi wa JUMUWATA. Mwanablogu atakaye kugombea ukatibu, anahitajika kuwakilisha jina na picha yake . Atatakiwa ajieleze ni kwanini anafikiria yeye ni bora kuongoza JUMUWATA. Baada ya hapo atasubiri upigaji kura kama utakavyo andaliwa na kamati maalumu ya uchaguzi. Wapiga kura ndio waamuzi wa mwisho wa uchaguzi.
32.Wakati na muda wakushika madaraka ya Ukatibu.
Muda wa uongozi ni miaka miwili. Katibu anaweza kujiudhuru au kuenguliwa kwa mujibu wa katiba.
33.Masharti ya kazi ya Ukatibu.
Katibu hataruhusiwa kuwepo katika kamati ya uchaguzi iwapo ananuia kugombea tena uongozi wa JUMUWATA. Ni mtunzaji wa JUMUWATA, hatakiwi kuigeuka JUMUWATA akiwa ofisini. Kuigeuka JUMUWATA ni kujitoa kwake kwenye uongozi wa JUMUWATA.
34.Kiapo cha Katibu wa JUMUWATA
Katibu ataapishwa kwa kiapo cha kukiri kufuata katiba ya JUMUWATA.
SEHEMU YA TATU
MUWEKA HAZINA:
35.Muweka Hazina
Ni muhusika mkuu wa maswala yote yahusuyo fedha za JUMUWATA.
36.Kazi na Mamlaka yake katika JUMUWATA
* Nimtunza fedha na rekodi zote zihusianazo na fedha za JUMUWATA.
* Ni msimamizi wa shughuli zote za ukusanyaji wa michango na shughuli nyingine zote zihusianazo na uingizaji fedha kwa JUMUWATA.
* Ni mkuu wa maswala yakutambua vyanzo vya fedha na kusimamia mipango ya upatikanaji wa michango au fedha na mali hizo.
* Msimamizi wa akaunti za JUMUWATA. Anahakikisha na kuweka sawa maswala ya mapato na matumizi a JUMUWATA yanaenda ipaswavyo katika kutimiza shughuli na miradi ya JUMUWATA.
* Ni muhusika wakutengeneza repoti ya fedha, kwenye mkutano mkuu au hata kwa kikundi cha WANAJUMUWATA itokeapo wapo watakao kujua maswala ya mapato na matumizi ya JUMUWATA.
* Atawajibika kuwakilisha ripoti ya mapato na matumizi pia mwishoni mwa kipindi chake cha uongozi au akiwa anajiudhuru kabla ya muda wa uongozi wake kufika.
* Anahakikisha kuwa mwenyekiti anajua hali ya kifedha ya JUMUWATA mara kwa mara.
* Ataandaa bajeti ya JUMUWATA kutokana na yale JUMUWATA itakayopanga kufanya kwa kipindi cha mwaka.
37.Uchaguzi wa Muweka Hazina
Uchaguzi wa muweka hazina utafanyika kwa kawaida pamoja na uchaguzi mkuu wa viongozi wengine.Uchaguzi wadharura waweza kufanyika pale muweka hazina ajiudhurupo au kutakiwa kujiengua kutokana na kukiuka maadili ya JUMUWATA.
38.Sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Muweka Hazina
Muweka hazina wa JUMUWATA ni mwanajumuwata yeyote mwenyeblogu atakaye gombea , mwenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi. Muweka hazina anatakiwa aonyeshe moyo wa kutaka kuendeleza JUMUWATA. Aonyeshe kuwa anauwezo wa kuendesha jumuiya hasa katika maswala ya fedha na uongozi kwa ujumla. Ni yule atakayeshinda kwa kura halali za wanajumuiya.
39.Haki ya kuchaguliwa tena
Muweka hazina anahaki ya kugombea tena kiti hicho kihalali kama wanajumuiya hawana kipingamizi na wanaridhika na kazi aifanyayo.
40.Utaratibu wa uchaguzi wa Muweka Hazina
Uchaguzi wa Muweka hazina utafuata taratibu za kawaida za uchaguzi wa JUMUWATA. Mwanablogu atakaye kugombea uweka hazina, anahitajika kuwakilisha jina na picha yake . Atatakiwa ajieleze ni kwanini anafikiria yeye ni bora kuongoza JUMUWATA. Baada ya hapo atasubiri upigaji kura kama utakavyoandaliwa na kamati maalumu ya uchaguzi. Wapiga kura ndio waamuzi wa mwisho wa uchaguzi.
41.Wakati na muda wakushika madaraka ya Uweka Hazina
Muda wa uongozi ni miaka miwili. Muweka hazina anaweza kujiudhuru au kuenguliwa kwa mujibu wa katiba.
42.Masharti ya kazi ya Uweka Hazina
Muweka hazina hataruhusiwa kuwepo katika kamati ya uchaguzi iwapo ananuia kugombea tena uongozi wa JUMUWATA. Ni mtunzaji wa JUMUWATA, hatakiwi kuigeuka JUMUWATA akiwa ofisini. Kuigeuka JUMUWATA ni kujitoa kwake kwenye uongozi wa JUMUWATA.
43.Kiapo cha Muweka Hazina
Muweka hazina ataapishwa kwa kiapo cha kukiri kufuata katiba ya JUMUWATA.
SEHEMU YA NNE
44.Kamati za JUMUWATA
a. Kamati ya harakati
Kamati ishughulikiayo utangazaji na upelekaji wa elimu na mafunzo yawafaayo wananchi yapatikanayo katika blogu za JUMUWATA kufikia jamii. Kamati hii itashughulikia miradi itokanayo na Jumuwata kufanyiwa kazi katika maeneo yagusayo jamii moja kwa moja .(Mfano :kutoa mafunzo madarasani na katika jamii kwa njia ya uso kwa uso au kwa kutumia vitabu,pamfleti,videonk.,kuhudumia watoto wa mitaani, kuhamasisha usafi, kupanda miti nk.).
b. Kamati ya Ufundi na teknolojia
Kamati hii huhusika na:
* Ufundi utumikao kuboresha blogu na pia mambo mapya ya teknolojia yawezayo kuboresha blogu za wanaJumuwata.
* Itakuwa na majukumu ya kuwezesha mikutano ya JUMUWATA katika mtandao.
* Kusaidi kushauri waanzao kublogu
* Kutupa taarifa mpya za tekinolojia huru ambazo zitasaidia kuboresha blogu zetu
* Kupeleka elimu ya blogs mashuleni nk ikishirikiana na kamati ya harakati.
* Kutengeneza na kuhudumia kikusanya habari(aggregator)
* Kuunda na kuimarisha tovuti ya jumuiya.
* Kutoa elimu ya kutengeneza blogu kwa atakayependa
c. Kamati ya Mahusiano na vyombo vya habari.
Kamati hii itahusika na kujenga uhusiano wa Wanablogu wa JUMUWATA na vyombo vya habari, vya Tanzania na Dunia. Itahusika kuandaa habari muhimu ambazo JUMUWATA inapendelea ziwafikie Wananchi kwa kutumia vyombo vingine vya habari kama vile TV,na magazeti.Itahusika kuhakikisha jina la JUMUWATA halichafuliwi na vyombo vingine vya habari.
d. Kamati ya Maadili na Ubora wa Blogu (Kamati ya picha)
Kamati hii itashughulikia uboreshaji wa blogu za JUMUWATA hasa katika maswala ya matumizi ya picha na uboreshaji wa taaluma ya picha , video na mengineyo yahusuyo uboreshaji wa blogu ili kuzipa nguvu zaidi katika uelimishaji jamii na pia kurahisisha ujumbe kufikia jamii.
e. Kamati ya sheria na Utunzaji wa maadili ya JUMUWATA
Kamati hii huhakikisha kuwa sheria na maadili ya JUMUWATA yanafuatwa na wanaJUMUWATA. Pia hufuatilia na kuweka wazi maswala ya kisheria ambayo yanaweza kumkumba mwanablogu. Itahusika pia na kuandaa hatua za kuwaengua viongozi na wanajumuwata kama wanakiuka maadili na sheria zichungazo JUMUWATA.
f. Kamati ya uenezi na uhamasishaji
Kamati hii inashughulikia maswala ya kupata wanablogu wapya na kusaidia kuwaamsha wanablogu wanaolala na kuacha kublogu. Kamati hii itahusika pian a kuelezea manufaa ya kublogu kwa jamii.
g. Kamati maalumu ya uchaguzi
Kamati hii itashughulikia maswala yote ya uchaguzi wa viongozi wa JUMUWATA. Itahusika pia na mapendekezo ya uchaguzi wa miradi itakayotakiwa kupewa kipaumbele na JUMUWATA katika kipindi husika.
45.Uteuzi wa wanaKAMATI
Wanakamati watagombea uanakamati kwa kuwasilisha majina na picha zao na picha zao kwa wanajumuwata kuwakubali. Wanakamati pia wanaweza kupendekezwa na wanajumuwata waaminio uwezo wao katika kushughulikia kamati zihusikazo.
46.Sifa za kuchaguliwa kuwa Mwanakamati.
Mwanakamati anaweza kuwa ni mwanablogu mwenyeblogu au ambaye hana. Ambaye hana blogu anatakiwa awe anatambulika na anajulikana kwa jina lake halisi. Anatakiwa aonyeshe moyo wa kutaka kuendeleza JUMUWATA. Aonyeshe kuwa anauwezo wa kuendesha maswala ya kamati na anaaminika.
47.Haki yakuchaguliwa tena
Mwanakamati anahaki yakupendekeza au kupendekezwa jina lake tena kushika uwanakamati .Wanajumuwata kwa kura wataamua.
48.Masharti ya kazi za Uwanakamati.
Mwanakamati hataruhusiwa kuwepo katika kamati ya uchaguzi iwapo ananuia kugombea uongozi wa JUMUWATA. Ni mtunzaji wa JUMUWATA, hatakiwi kuigeuka JUMUWATA akiwa ofisini. Kuigeuka JUMUWATA ni kujitoa kwake kwenye uongozi wa JUMUWATA.
49.Kiapo cha Mwanakamati
Mwanakamati ataapishwa kwa kiapo cha kukiri kufuata katiba ya JUMUWATA.
50.Wakati na muda wakushika uwanakamati
Muda wa uongozi ni miaka miwili. Mwanakamati anaweza kujiudhuru au kuenguliwa kwa mujibu wa katiba.
SEHEMU YA TANO
MENGINEYO KATIKA UTARATIBU WA SHUGHULI ZA JUMUWATA:
51.Hazina ya JUMUWATA
Nchi akaunti za JUMUWATA zitakapo kuwepo.
Mali nyingine za JUMUWATA
52.Vianzo vya pato la JUMUWATA
* Michango ya watu binafsi
* Michango ya wanablogu
* Michango kutoka katika mashirika
* Michango kutoka serikalini
* Zawadi
53.TARATIBU za uhakiki wa fedha za JUMUWATA
* ODITA
Odita atapendekezwa kwenye kikao kikuu na atakuwa ni mtu asiye husika moja kwamoja na JUMUWATA
54.Vikao vya JUMUWATA
* Vikao vikuu
* Vikao vya dharura
#Hivi ni vikao vitakavyo itishwa pale mambo muhimu yatakapojitokeza kabla ya tarehe ya mkutano mkuu kufika.
* Vikao vya kamati
Vikao vya kamati vitafanyika na kuandaliwa na wanakamati wa kamati husika .Wanakamati watatakiwa kufanya vikao kabla ya vikao vikuu vya JUMUWATA ilikufikisha maswala ya kamati katika vikao vikuu kujadiliwa.
55.Tarehe muhimu za JUMUWATA
56.Zawadi kwa bloggers
* Blogu bora ya kisiasa
* Blogu bora ya kifalsafa na maudhui ya kimaisha
* Blogu bora ya sanaa
* Blogu bora ya picha
* Blogu bora ya fasheni
* Blogu bora ya marafiki wa JUMUWATA
* Blogu bora ya maadili ya kiufundi na teknolojia
* Blogu bora ya maswala ya Kilimo
* Blogu bora ya maswala ya jamii
* Blogu mpya bora
* Blogu ya mwaka
* Bloga wa mwaka
* Blogu bora ya mapishi
* Blogu bora ipendezayo
* Blogu bora kiufundi
SEHEMU YA SITA
57. UVUNJWAJI WA JUMUWATA:
a.JUMUWATA itavunjwa na kikao kitakacho wasilishwa na zaidi ya wanajumuwata zaidi ya robo tatu wenye kuamua kuwa JUMUWATA hainamanufaa kuendelea.
b. Baada ya kuvunjwa mali zote za JUMUWATA zitasambazwa kwa mirad isiyobinafsi yenye kufaidisha jamii kwa ujumla.
58. UHALALI.
a.Mikataba na vyeti vyote muhimu vitahitaji sahihi za viongozi wawili. Kutokana na wanajumuwata kusambaa duniani. Mwenyekiti atapewa uwezo wakuchagua viongozi ambao wanapatikana katika ngazi tatu za JUMUWATA kuweka sahihi katika mikataba au vyeti muhimu vya JUMUWATA.